MWANANYAMALA RRH YAADHIMISHA SIKU YA WATOTO WANAOZALIWA KABLA YA WAKATI KWA KUFANYA MATEMBEZI YA HISANI
Posted on: November 17th, 2023MWANANYAMALA RRH YAADHIMISHA SIKU YA WATOTO WANAOZALIWA KABLA YA WAKATI KWA KUFANYA MATEMBEZI YA HISANI
Katika Kusheherekea Maadhimisho Siku ya Watoto wanaozaliwa Kabla ya wakati kwa mwaka 2023, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala imeungana na watu wote duniani kuadhimisha siku hiyo kwa kufanya matembezi ya hisani yenye lengo kupeleka ujumbe kwa jamii kuwa watoto waliozaliwa kabla ya muda wananafasi ya kukua vyema kama watoto wengine.
Maadhimisho hayo yamekwenda sambamba na kutoa elimu kwa umma kuhusu visababishi vinavyopelekea watoto kuzaliwa kabla ya wakati na namna ya kuwatunza watoto hao pamoja na utoaji wa zawadi kwa baadhi ya mama (Surrogate mothers) na baadhi ya watoto waliozaliwa kabla ya wakati katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Dr.Macrina Kato, Daktari Bingwa wa Watoto na Mkuu wa Idara ya Watoto Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala ameishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mh. Rais Dr. Samia Suluhu Hassan pamoja Waziri wa Afya Mh. Ummy Mwalimu kwa jitihada za dhati na endelevu katika kuhakikisha huduma za watoto wachanga zinaboreshwa.
"Tunashukuru pia Uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mwananyamala chini ya Mganga Mfawidhi wetu Dr Zavery Benela kwa kuwa pamoja nasi katika jitihada zote za kuokoa maisha ya watoto wachanga. Kipekee tunawashukuru NEST360 chini ya IFAKARA HEALTH INSTITUTE kwa kuwa bega kwa bega nasi katika kuendelea kuboresha huduma za watoto wachanga na kuweza kufanikisha siku hii muhimu." amesema Dr. Kato.
Maadhimisho ya Siku ya Watoto Wanaozaliwa Kabla ya Wakati huadhimishwa Novemba 17 kila mwaka, na kwa mwaka huu maadhimisho haya yamebeba kaulimbiu isemayo "Hatua Kidogo, Faida Kubwa" na kusisitiza muambatano wa ngozi kwa ngozi baina ya mama/mlezi na mtoto aliyezaliwa kabla ya wakati ili kuhakikisha watoto hao wanapata afya na kukua vyema.