DKT MOLLEL ARIDHISHWA NA UBORA WA HUDUMA HOSPITALI YA MWANANYAMALA

Posted on: November 19th, 2023

DKT MOLLEL ARIDHISHWA NA UBORA WA HUDUMA HOSPITALI YA MWANANYAMALA

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel   ameridhishwa na hali ya utoaji huduma bora kwa wananchi wanaofika kupata huduma katika hospitali ya Rufaa ya mkoa Mwananyamala.

Dkt.Mollel amebainisha hayo  leo Jijini Dar es Salaam  alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma za afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mwananyamala ambapo ameupongeza uongozi wa Hospitali hiyo na kufurahishwa na utolewaji wa huduma za Dialysis kwa wagonjwa wa figo, ubora wa jengo la dharura  na usafi wa mazingira wa Hospitali ya hiyo

"Nimeingia jengo lenu la Emergency, hakuna harufu za ajabu, usafi ni asilimia 98", amekiri Dkt.Mollel 

Dr. Mollel amewataka viongozi wa hospitali zote za rufaa za mkoa wa Dar es Salaam kuendelea kusimamia vizuri  watumishi wanaowaongoza na watumishi kuendelea kuwatii viongozi waliopewa dhamana ya kuwaongoza na ametaka hospitali zote za rufaa za mkoa kujiandaa kukabiliana na matukio ya mwisho wa mwaka na athari za mvua endapo itahitajika kutoa huduma za dharura.

Naye Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala mbali na kumshukuru  Naibu Waziri wa Afya kwa ujio wake, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dr. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia  Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala kiasi cha Sh. Bilion 3.2 ambazo ni fedha za mradi wa UVIKO-19, ambazo zimesaidia ujenzi wa jengo la dharura na ajali, ujenzi wa jengo la ICU na uboreshaji wa huduma za mionzi katika Idara ya Radiolojia, ununuzi wa vifaa tiba katika maeneo hayo ambapo ujenzi na maboresho mengi yamechangia Hospitali ya Mwananyamala kuwa katika viwango ilivyo kwa sasa.