DR. HONGO ATOA ELIMU KUHUSU MADHARA YA MATUMIZI YA TUMBAKU KUELEKEA SIKU YA MATUMIZI YA TUMBAKU DUNIANI.
Posted on: May 26th, 2025
Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Matumizi ya Tumbaku Duniani Mei 31 2025, Daktari wa afya ya akili na uraibu wa dawa za kulevya wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala, Dkt. Jofu Hongo, ametoa elimu kuhusu madhara ya kiafya yatokanayo na matumizi ya tumbaku kwa muda mrefu.
Akizungumza kupitia kipindi cha #Pilikapilika cha kituo cha redio cha East Africa Radio leo, Dkt. Hongo amesisitiza umuhimu wa jamii kuelewa athari zinazotokana na matumizi ya tumbaku na kuchukua hatua madhubuti za kujiepusha nayo.
Dkt. Hongo ameeleza kuwa tumbaku inaathiri mifumo mbalimbali ya mwili wa binadamu, ikiwa ni pamoja na mfumo wa upumuaji, moyo na mishipa ya damu, pamoja na afya ya uzazi.
Aidha, Dkt. Hongo ameongeza kuwa tumbaku huongeza hatari ya kupata magonjwa sugu kama vile saratani ya mapafu, kiharusi, na maradhi ya moyo. Amesisitiza kuwa kemikali hatarishi zilizopo kwenye tumbaku si tu huathiri watumiaji wa moja kwa moja, bali pia huwadhuru watu wanaovuta moshi wa tumbaku kwa njia ya pili (secondhand smoke), wakiwemo watoto na wazee.
Katika ujumbe wake kwa jamii, Dkt. Hongo ameitaka jamii kuwa na mwamko wa kupambana na matumizi ya tumbaku kwa kuelimishana, kusaidiana kuacha matumizi, na kuunga mkono juhudi za serikali na taasisi nyingine katika kupunguza matumizi ya bidhaa hiyo hatarishi. Amesema kuwa mapambano dhidi ya tumbaku yanahitaji mshikamano wa pamoja ili kulinda afya ya kizazi cha sasa na kijacho.
Maadhimisho ya Siku ya Matumizi ya Tumbaku Duniani hufanyika kila mwaka tarehe 31 Mei, yakilenga kuelimisha jamii kuhusu athari za tumbaku na kuchochea utekelezaji wa sera na sheria zinazolenga kupunguza matumizi ya tumbaku duniani kote.