JAMII YAELIMISHWA KUHUSU DALILI HATARI ZA MAGONJWA MBALIMBALI YA TUMBO

Posted on: June 15th, 2025

Jamii imetakiwa kuwa makini na dalili mbalimbali za magonjwa ya tumbo, na kuchukua hatua mapema za kiuchunguzi wa kitabibu kabla ya kusababisha changamoto kubwa zaidi.

Akizungumza kupitia katika kipindi #Pilikapilika kinachorushwa na East Africa Radio, Daktari wa magonjwa ya ndani katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala, Dkt. Julius Majenga amesema dalili hizo za hatari zinazoambata na maumivu ya tumbo ni kama vile kupata kiungulia mara kwa mara, kutopata choo au kupata choo kwa shida, kuongezeka kwa mapigo ya moyo na kizunguzungu, zinaweza kuwa viashiria vya magonjwa hatari ya mfumo wa chakula hivyo jamii haitakiwi kupuuza dalili hizo.




Aidha Dkt. Julius ameeleza kuwa baadhi ya sababu kuu zinazosababisha tumbo kuuma ni pamoja na ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi au viungo vikali, msongo wa mawazo, matumizi holela ya dawa, na dawa za maumivu, ulevi, na maambukizi ya bakteria aina ya Helicobacter pylori. 


Katika hatua nyingine, Dkt. Julius amehimiza jamii kuchukua hatua mapema kwa kufanya uchunguzi wa kitabibu mara wanapohisi mabadiliko yoyote ya kiafya kwenye mfumo wa mmeng’enyo wa chakula.



“Watu wengi hufika hospitalini hali ikiwa imekuwa mbaya sana. Ni muhimu kuchukua hatua mapema ili kuepusha madhara makubwa yanayoweza kupatikana ikiwemo magonjwa ya Figo na Ini” amesema Dkt. Julius.

Kwa upande mwingine, alitoa wito kwa jamii kuzingatia ulaji wa chakula bora chenye nyuzinyuzi (fiber), kunywa maji ya kutosha, kuepuka ulaji wa vyakula vya haraka (fast foods), pamoja na kupunguza matumizi ya pombe na sigara. Pia alisisitiza umuhimu wa kufanya mazoezi mara kwa mara kama sehemu ya kinga dhidi ya magonjwa ya tumbo.