MKURUGENZI WA TIBA WIZARA YA AFYA APONGEZA UBORESHAJI HUDUMA ZA DIALYSIS KATIKA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA MWANANYAMALA

Posted on: August 1st, 2023


Mkurugenzi wa Tiba kutoka Wizara ya Afya Prof. Paschal Ruggajo ameupongeza uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala kwa kuhakikisha huduma za Dialysis zinatolewa kwa ubora na viwango vinavyotakiwa.
Prof. Ruggajo ameyasema hayo leo alipofanya ziara katika Hospitali hiyo yenye lengo la kukagua huduma zinazotolewa na Kitengo cha Dialysis na uwezo wake wa kutoa huduma hizo ambapo amekiri kuridhishwa na utoaji huduma unaofanywa na Kitengo hicho.

Nchi yetu imepiga hatua kubwa katika Ukanda wa Afrika Mashariki katika utoaji wa huduma za Dialysis, nimeridhika sana na huduma zitolewazo hapa na niseme tu Mwananyamala ya sasa si ya zamani.

Prof. Ruggajo ametoa wito kwa uongozi kuhakikisha ubora wa utoaji huduma kwa wateja unaendelezwa kwani Serikali imeboresha mazingira,  miundombinu na Vitendea kazi ili watanzania wapate huduma bora za afya.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala Dkt. Zavery Benela amemshukuru Mkurugenzi huyo kwa ujio wake na kumuhakikishia kuwa, Watendaji na Watoa Huduma Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala wataendelea kutoa huduma kwa ufanisi, weledi na kwa kuzingatia viapo vyao.