MTULIA, MAKONGO SEKONDARI WAMUENZI BABA WA TAIFA KIAINA MWANANYAMALA HOSPITALI

Posted on: October 10th, 2019


Mbunge wa jimbo la kinondoni Abdallah Mtulia ameungana na uongozi wa Shule ya Sekondari Makongo katika kumuenzi Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Mbunge huyo amefanya hivyo leo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala. Ni tukio la aina yake kwani mbunge huyo pamoja na wanafunzi hao wameshiriki kwa pamoja katika zoezi la kufanya usafi wa mazingira ya Hospitali. Pia walimu wa Shule hiyo ambao wengi wao ni askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wamejumuika pamoja na wanafunzi wao katika zoezi hilo la usafi.

Pamoja na kufanya usafi pia wameshiriki katika zoezi la upandaji wa miti na maua katika baadhi ya maeneo ya Hospitali. Zoezi hilo limeenda sambamba kwa ushirikiano mkubwa wa uongozi wa Hospitali hiyo ukisimamiwa na Kaimu Mganga Mfawidhi Dr. Isdory Kiwale.

                                                                                                                                            Picha kwa hissani ya Merina Makasi

Akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo Mbunge huyo amewapongeza wanafunzi hao kwa moyo wao wa kizalendo kwani wamejito katika kuhakikisha mazingira yanakuwa katika hali nzuri kwa kuyasafisha na kupanda miti na maua.

Baada ya zoezi la usafi na upandaji wa miti wanafunzi hao pamoja na walimu wao wamechangia damu ambapo kwa pamoja zilipatikana units 42.

Mbunge Mtulia hakusita kuumwagia sifa uongozi wa Shule ya Sekondari Makongo na wanafunzi wao kwa jinsi walivyojitoa.

“Tunafanya yote haya kumuenzi Mwalimu Nyerere, alituhimiza upendo, umoja, uzalendo na kusaidiana, na akatuletea sera ya ujamaa na kujitegemea. Huu ni mfano wa kuigwa, tuendelee kumuenzi kwa kufanya yale aliyotuagiza, alifanya mambo mengi mazuri enzi za uhai wake, alijenga viwanda vidogo na vya kati na hospitali mbalimbali ikiwamo hii ya Mwananyamala. Alitutengenezea Majeshi madhubuti mfano hili la JWTZ tangu 1964 alipolianzisha limekuwa nguzo muhimu kwetu, tunaheshimika hata majirani (nchi zingine),wanatujali na tupo salama kwa sababu Jeshi letu lipo madhubuti,” amesema Mtulia.

Akizungumza, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Makongo, Kanali Yuda Kitinya, amesema; 

“Tumefanya hivi lengo letu hasa ni kuwafundisha vijana wetu uzalendo, wafahamu kwamba wana jukumu la kujitoa kwa ajili ya jamii inayowazunguka.

Naamini wataendelea kujitolea kwa jamii, sisi ni chachu tu, kama chumvi kwenye jamii, shule nyingine nazo ni vema waige mfano kwetu, wajitolee kwa jamii.”

Kaimu Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Isdory Kiwale, ameshukuru kwa mchango ambao umetolewa na Shule hiyo, kwa kusema

“Tunashukuru sana, huu ni mchango mkubwa kwetu, kujitolea damu ni uzalendo, nawasihi watanzania wengine nao waige mfano huu mzuri, wajitolee, kuchangia damu kwani inahitajika ili kusaidia kuokoa maisha ya wagonjwa wenye uhitaji.”