TAASISI YA JAI, HOSPITALI YA MWANANYAMALA WATOA HAMASA KUELEKEA ZOEZI LA UCHANGIAJI DAMU LITAKALOANZA AGOSTI 14 HADI 16, 2025
Posted on: August 10th, 2025
Mapema leo kupitia kipindi cha #Hello Tanzania cha Uhuru Fm, Taasisi ya JAI Wilaya ya Kinondoni kwa kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala wametoa wito kwa wananchi wa Jiji la Dar es Salaam na maeneo jirani kujitokeza kwa wingi kushiriki katika zoezi la uchangiaji damu litakalofanyika Hospitalini hapo kuanzia Agosti 14 hadi 16 2025.
Akizungumza katika mahojiano hayo, Amir wa Taasisi ya JAI, Khamis Mmanga, amesema maandalizi yamekamilika kuelekea zoezi hilo na lengo ni kusaidia kuokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji damu, hasa kwa kuzingatia misingi ya Imani na Utu.
Akieleza kuhusu sifa za mchangia damu, Mtaalamu wa Maabara na Mhamasishaji wa zoezi hilo Lewis Mwandemani, ameeleza kuwa mchagiaji damu anatakiwa kuwa na afya njema, mwenye umri kati ya miaka 18 na 60, na uzito usiopungua kilo 50.
"Tunawashauri wananchi wajitokeze kwa wingi na bila hofu wala wasiwasi wowote, mahitaji ya damu ni makubwa kutokana na idadi ya wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo kila siku". Ameeleza Lewis.
Kwa upande wake Afisa Uhusiano na Mawasiliano wa Hospitali ya Mwananyamala, Bw. Frolian Godwin, amesema Hospitali imejiandaa kikamilifu kuhakikisha kuwa zoezi hilo linafanikiwa na maandalizi yanayojumuisha upatikanaji wa vifaa vya kutosha, wataalamu wa afya, na maeneo maalum ya kupokelea wachangiaji yamekamilika.