VIONGOZI KUTOKA WIZARA YA AFYA ZANZIBAR WAVUTIWA NA HUDUMA YA MAMA NA MTOTO HOSPITALI YA MWANANYAMALA.

Posted on: July 13th, 2025

Baadhi ya viongozi kutoka Wizara ya Afya Zanzibar leo Julai 14, 2025 wametembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kujifunza namna huduma za mama na mtoto zinavyoboreshwa ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi, ziara hiyo ikiwa ni sehemu ya juhudi za kubadilishana uzoefu na kuimarisha mifumo ya afya baina ya Tanzania Bara na Zanzibar.


Katika ziara hiyo, viongozi hao wamepata nafasi ya kutembelea vitengo mbalimbali vinavyohudumia akinamama wajawazito na watoto wachanga, wakifuatilia kwa karibu namna hospitali ya Mwananyamala inavyotekeleza miongozo ya kitaifa ya afya ya uzazi salama.

Akizungumzia baada ya kujionea huduma hizo Bi Najma Abdalla Ali ambaye ni Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar, ameonesha kuridhishwa na namna huduma zinavyotolewa kwa ufanisi, zikiwemo huduma za dharura kwa mama mjamzito, upatikanaji wa dawa, na ushirikiano wa karibu kati ya wataalamu wa afya.


“Tumejifunza mambo mengi muhimu kutoka Hospitali ya Mwananyamala, hasa kwenye mifumo ya ufuatiliaji wa huduma kwa mjamzito hadi kujifungua. Tunaamini maarifa haya yatasaidia kuboresha huduma Zanzibar na kuchangia katika kupunguza vifo vya mama na mtoto,” ameeleza Bi Najma.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala, Dkt. Zavery Benela, amesema ujio wa viongozi hao ni fursa ya kujifunza pande zote mbili. 


“Tumefurahi sana kupokea ugeni huu, kwani hata sisi kama hospitali tumejifunza kutoka kwao kuhusu baadhi ya mbinu za usimamizi wa huduma za afya wanazotumia huko Zanzibar hasa wanavyoweza kuwasaidia kinamama wajawazito wanaopata changamoto ya kupungukiwa damu” amesema Dkt. Benela.



Kadhalika, viongozi hao wameambatana na wataalamu wa utafiti kutoka Taasisi ya Afya ya Ifakara (Ifakara Health Institute – IHI), ambao wameshiriki kubadilishana uzoefu kuhusu tafiti zinazosaidia kuboresha huduma za afya ya uzazi nchini.