WANAUME RUKSA KUAMBATANA NA WAKE ZAO WAKATI WA KUJIFUNGUA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA MWANANYAMALA.
Posted on: May 19th, 2025
WANAUME RUKSA KUAMBATANA NA WAKE ZAO WAKATI WA KUJIFUNGUA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA MWANANYAMALA.
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala, imeendeleza mapinduzi chanya katika utoaji wa huduma za afya ya uzazi kwa kuendeleza huduma ya kuruhusu wanaume kuambatana na wake zao katika wodi za kujifungua. Hatua hii inafuatia maboresho makubwa yaliyofanyika katika miundombinu ya wodi hizo, ikiwa ni sehemu ya dhamira ya Serikali kuhakikisha hospitali hiyo inatoa huduma bora, za kisasa, na zenye usiri kwa mama na mtoto.
Pamoja na kuwa katika jamii nyingi, jukumu la uzazi limekuwa likihusishwa zaidi na wanawake pekee, hata hivyo Hospitali ya Rufaa Mwananyamala imeuvunja mwiko huo kwa kutambua umuhimu wa ushiriki wa mwanaume katika safari ya uzazi ambapo sasa, si tu wanaume bali pia ndugu wa karibu wanaoridhiwa na mjamzito wanaruhusiwa kuwa sehemu ya mchakato wa kujifungua.
Je hili lina Faida gani kwa Mama na Mtoto?
Baadhi ya tafiti mbalimbali za kitabibu na kijamii zimeonesha wazi kuwa uwepo wa mtu wa karibu wakati wa kujifungua huchangia kwa kiasi kikubwa katika kupunguza maumivu ya kihisia na hata kimwili kwa mama. Wanawake wengi walioshiriki katika huduma hii wameeleza kuwa walihisi faraja, ujasiri, na msaada mkubwa kutoka kwa wenza wao au ndugu waliokuwa nao. Pia, hali hii huchangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha mahusiano ya kifamilia, kupunguza mkazo wa mjamzito, na kusaidia maamuzi ya haraka yanayohitaji ridhaa ya familia.
Kwa upande wa mtoto anayezaliwa, huduma hii inasaidia kuimarisha mazingira salama na yenye utulivu wakati wa kuzaliwa. Mama anapokuwa mtulivu na mwenye amani, hali hiyo huongeza uwezekano wa kujifungua kwa mafanikio bila hitaji la upasuaji au changamoto nyingine za kiafya.
Kwa upande mwingine, huduma hii pia imeleta mafanikio katika kuongeza elimu ya afya ya uzazi miongoni mwa wanaume. Kupitia kushiriki kwao moja kwa moja, wanajifunza kwa vitendo changamoto, hatua, na mahitaji halisi ya uzazi salama. Hii huchangia kuwaweka tayari kusaidia wake zao hata baada ya kujifungua, ikiwa ni pamoja na malezi ya mtoto mchanga, lishe, na afya ya mama katika kipindi cha baada ya kujifungua.
Hata hivyo, ili kuhakikisha huduma hii inatekelezwa kwa ufanisi, Hospitali ya Rufaa Mwananyamala imefanya maboresho ya kimazingira kama vile kuongeza nafasi katika vyumba vya kujifungulia, kuweka vitanda vya kisasa, pamoja na kuimarisha faragha na usalama wa mjamzito na kuimarishwa kwa mafunzo ya ndani kwa watumishi.
Pia, hatua ya kumruhusu mama mjamzito kuchagua mwenyewe mtu wa kuambatana naye ni msingi wa huduma inayozingatia haki, usawa, na ridhaa ya mgonjwa.
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala inatoa wito kwa jamii kuunga mkono huduma hii na kuitumia ipasavyo. Wanaume wanahimizwa kujitokeza kushiriki kikamilifu katika kipindi hiki muhimu cha maisha ya familia yao. Aidha, jamii kwa ujumla inapaswa kuondokana na mila potofu zinazoona kuwa kujifungua ni kazi ya wanawake pekee, na badala yake kujenga mshikamano wa kifamilia unaoanzia tangu ujauzito hadi malezi ya mtoto.
Kwa maelezo zaidi kuhusu huduma hii, tembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala au wasiliana nasi kupitia tovuti rasmi au mitandao yetu ya kijamii.