WATUMISHI HOSPITALI YA MWANANYAMALA WAJENGEWA UELEWA KUHUSU MATUMIZI SAHIHI YA VYOMBO VYA HABARI

Posted on: July 15th, 2025

Watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala leo Julai 16, 2025 wamepatiwa elimu juu ya matumizi sahihi ya vyombo vya habari kwa lengo la  kuwajengea uwezo wa kuwasiliana kwa ufanisi na jamii kuhusu huduma za afya zinazotolewa hospitalini, sambamba na umuhimu wa kufuata taratibu rasmi za utoaji wa taarifa.


Elimu hiyo imetolewa na Afisa Uhusiano na Mawasiliano wa hospitali hiyo Bw. Frolian Godwin, ambapo watumishi wamefundishwa namna bora ya kushiriki kwenye vipindi vya redio, televisheni, na majukwaa ya mtandaoni kwa ajili ya kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya afya kwa kutumia lugha rahisi, sahihi na ya kuvutia, ili kuwasaidia wananchi kuelewa huduma zinazotolewa na umuhimu wa kupata matibabu kwa wakati.

Akizungumza katika kikao hicho, Afisa Uhusiano ameeleza kuwa vyombo vya habari ni nyenzo muhimu katika kuelimisha jamii, kuondoa upotoshaji, na kujenga imani ya wananchi kwa taasisi za afya. 


“Tunapovitumia vyema vyombo vya habari, tunapanua wigo wa uelewa wa wananchi kuhusu huduma za kitabibu, haki zao, na namna bora ya kujikinga na magonjwa,” ameeleza Frolian.



Aidha, watumishi wametakiwa kuhakikisha wanazingatia misingi ya utoaji wa taarifa ikiwemo kupata idhini ya mawasiliano rasmi, kuwasilisha taarifa kwa usahihi na kuepuka kutoa taarifa zenye mgongano au zinazoleta hofu kwa jamii, kuzingatia maadili ya taaluma, umuhimu wa usiri wa taarifa za wagonjwa, na namna ya kujibu maswali ya waandishi wa habari kwa ufasaha.



Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mwananyamala, Dkt. Zavery Benela, amesema hospitali itaendelea kuboresha mifumo ya mawasiliano ya ndani na nje ili kuhakikisha kuwa jamii inapata taarifa sahihi kwa wakati.