WITO WA KUCHANGIA DAMU WATOLEWA KWA JAMII KUELEKEA MAADHIMISHO YA SIKU YA MCHANGIA DAMU DUNIANI JUNI 14, 2025.

Posted on: June 12th, 2025

Kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mchangia Damu Duniani yanayofanyika kila mwaka tarehe 14 Juni, wananchi wametakiwa kujitokeza kwa wingi kuchangia damu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwananyamala ili kusaidia kuokoa maisha ya watu wenye uhitaji wa damu.


Meneja wa Maabara ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala, Bw. Shauri Njama, ametoa wito huo akisisitiza umuhimu wa zoezi hilo kwa jamii nzima. Ameeleza kuwa mahitaji ya damu katika hospitali bado ni makubwa kutokana na ongezeko la wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo, hususan wanawake wajawazito, watoto wachanga, waathirika wa ajali, na wagonjwa wanaopata upasuaji au matibabu ya saratani.

"Tunawahamasisha wananchi wote wa Jiji la Dar es Salaam na maeneo jirani kujitokeza kuchangia damu, si tu kwa ajili ya kusherehekea siku hii muhimu duniani, bali pia kama sehemu ya kutoa mchango wa kweli wa kuokoa maisha ya Watanzania wenzetu wanaohitaji damu, kwakuwa damu ni uhai," amesema Bw. Njama.


Kuchangia damu ni tendo la kiutu na la huruma linaloweza kuokoa maisha ya mtu mwingine. Kila tone la damu linaweza kumsaidia mgonjwa kurejea katika hali yake ya kawaida na kuendelea na maisha. Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, chupa moja ya damu inayotolewa na mchangiaji inaweza kusaidia hadi watu watatu tofauti, jambo linaloonyesha thamani kubwa ya mchango huo.


Miongoni mwa sifa za mchangia damu ni pamoja na kuwa na umri wa kuanzia miaka 18 hadi 65, kuwa na uzito wa angalau kilo 50, na afya njema bila kuwa na dalili za maradhi kama malaria, shinikizo la damu au magonjwa ya kuambukiza kama UKIMWI na homa ya ini. Aidha, mchangiaji hapaswi kuwa ametumia dawa au pombe muda mfupi kabla ya kuchangia, na kwa wanawake, anapaswa kuwa si mjamzito wala anayenyonyesha.


Maadhimisho ya mwaka huu yanalenga kuonyesha umuhimu wa mchango wa hiari wa damu na kutambua mchango wa wachangia damu wa mara kwa mara ambao wanahakikisha damu salama inapatikana kwa wagonjwa. Wananchi wote wanahimizwa kushiriki kikamilifu katika siku hiyo, si tu kwa kuchangia damu, bali pia kwa kujifunza kuhusu umuhimu wa zoezi hilo.