Saratani

Posted on: February 23rd, 2020

Magonjwa ya Saratani

Saratani hutokea wakati sehemu ya mwili inapokua na kuongezeka bila utaratibu na kusababisha uvimbe. Kwa kawaida saratani huanza taratibu na huchukua muda kuonyesha dalili zozote. Pia dalili za awali haziambatani na maumivu hivyo kusababisha wagonjwa wengi kuchelewa kutafuta matibabu. 


Kila mwaka zaidi ya watu milioni 12 hugunduliwa kuwa na saratani ulimwenguni. Saratani inaua watu wengi zaidi kuliko jumla ya wote wanaokufa na UKIMWI, malaria na kifua kikuu. Lakini ni vizuri kujua ya kuwa kwa kila saratani tano zinazotokea mbili zinaweza kuzuilika na pia ingawaje saratani hazina tiba, nyingi zinaweza kuondolewa kabisa na zisirudi tena.


Mambo yanayochangia kuwepo magonjwa ya saratani

Asilimia 60 ya magonjwa yote ya saratani yanahusishwa zaidi na mtindo wa maisha ambao vipengele vyake ni ulaji, mazoezi ya mwili, matumizi ya pombe na tumbaku. Mambo mengine yanayochangia ni pamoja na virusi na bakteria, madini mazito, mionzi na sumu kadhaa.


Vyakula 

Vyakula huchangia kwa kiasi kikubwa saratani za kinywa na koo, matiti, tezi ya kiume, utumbo mpana, mapafu, tumbo, ini, kongosho na kizazi. Ulaji unaoweza kuchangia ni pamoja na:

Ulaji wa nyama nyekundu kupita kiasi 

Nyama zilizosindikwa 

Vyakula vilivyokuzwa kwa kemikali nyingi (k.m. mbolea), na  Vyakula vyenye mafuta mengi ambavyo huweza kusababisha uzito mwingi 

Vyakula vilivyoota ukungu, kwa mfano karanga.

 

Nyama Nyekundu 

Nyama nyekundu ni muhimu kwa binadamu, lakini ni tatizo inapoliwa zaidi ya nusu kilo kwa wiki. Ulaji wa nyama nyekundu kwa kiasi kikubwa unaongeza uwezekano wa kupata saratani ya utumbo mkubwa. Tafiti zimeonesha ya kuwa kula hadi nusu kilo kwa wiki haiongezi uwezekano wa kupata saratani lakini kila gramu 50 zinazoongezeka huongeza uwezekano wa kupata saratani kwa asilimia 15

 

Nyama Zilizosindikwa

Nyama zilizosindikwa pamoja na zile zilizohifadhiwa kwa kuongezwa chumvi, mafuta, kemikali au kukaushwa kwa moshi (k.m. nyama za kopo, soseji, na bekoni) zinaongeza sana uwezekano wa kupata saratani. Hakuna kiasi chochote cha nyama iliyosindikwa kinachoweza kutumika bila kuongeza uwezekano wa kupata saratani

 

Uzito Uliozidi 

Uzito uliozidi kiasi unamweka mtu kwenye hatari ya kupata magonjwa mengi sugu kwa mfano kisukari, msukumo mkubwa wa damu, magonjwa ya moyo, figo, na saratani za matiti, kongosho na kizazi. Utaratibu mzuri wa kula husaidia kupunguza uzito au kuzuia ongezeko kubwa la mwili.


Pombe na Tumbaku 

Matumizi ya pombe na tumbaku huchangia sana ongezeko la saratani za koo na mapafu. Hapa nchini ongezeko ni kubwa. Asilimia 90 ya wagonjwa waliopokelewa Hospitali ya Saratani ya Ocean Road walikua na historia ya kutumia vilevi vikali, tumbaku, pilipili kwa wingi na aina nyingine ya vitu vinavyosababisha saratani hii. Pombe inaongeza sana uwezekano wa kupata saratani hasa zile za koo, kinywa, ini na matiti.

 

Virusi na Bakteria 

Saratani za ini, mdomo wa mji wa mimba, mdomo, ngozi, tumbo, mfupa wa taya na kibofu cha mkojo.

 

Vyakula Vinavyopunguza Uwezekano wa Kupata Saratani

Vyakula vitokanavyo na mimea ni kinga nzuri ya kuzuia saratani. Kutumia zaidi vyakula vitokanavyo na mimea husaidia kuondoa uwezekano wa kupata saratani za aina mbalimbali. Inashauriwa kula angalau vipimo vitano vya mboga mbali mbali kila siku. Hakikisha katika kila mlo unatumia nafaka zisizokobolewa sana kama unga wa ngano usiokobolewa sana, unga wa dona, mchele wa brauni, ulezi kwani haukobolewi, na aina mbalimbali za mikunde kama maharage, kunde, choroko, mbaazi, n.k.


Mazoezi ya Mwili

Mazoezi ya mwili yawe sahemu ya maisha kila siku. Inashauriwa kufanya mazoezi ya mwili ya wastani kama vile kutembea haraka haraka angalau dakika 30 kila siku, na mwili ukishazoea ongeza hadi kufikia dakika 60 kila siku. Kama unafanya mazoezi ya nguvu sana basi iwe angalau dakika 30 kila siku. Punguza sana mtindo wa maisha ambao unakufanya uketi bila mazoezi kama vile kuangalia televisheni kwa muda mrefu. Tumia nafasi zote zilizopo za kuzoeza mwili kama vile kupanda ngazi badala ya kutumia lifti, kusaidia kazi za nyumbani, kutembea kwenda sokoni au dukani kama si mwendo mrefu, n.k.


Dalili za Awali za Magonjwa ya Saratani

Magonjwa mengi ya saratani hutibika yakigundulika mapema. Hivyo ni muhimu kumwona mapema mhudumu wa afya kila unapoona dalili zifuatazo:

  • Kukosa hamu ya kula 
  • Kupungua uzito bila sababu 
  • Uchovu bila ya kufanya kazi 
  • Uvimbe wa zaidi ya wiki tatu shingoni, kwapani, tumboni, ngizi au matiti 
  • Kubadilika kwa kawaida yako ya kupata choo (kufunga choo) 
  • Kutokwa na ute, maji maji au usaha ukeni 
  • Kutokwa na damu kwenye choo, mkojo, makohozi au pua 
  • Kwa wanawake, kutokwa na damu ukeni baada ya tendo la ndoa, baada ya kukoma mzunguko wa hethi, au nje ya mzunguko wa hedhi 
  • Shida au maumivi ukimeza chakula au vinyaji 
  • Kukohoa au sauti ya kukwaruza kwa zaidi ya wiki tatu 
  • Matiti kubadilika umbile, uvimbe, ngozi au kutoa maji maji 
  • Kukojoa mara nyingi zaidi ya kawaida yako au mkojo kutoka kwa shida


Aina za Saratani tutakazo zijadili hapa

  1.  TEZI DUME.
  2.  SARATANI YA SHINGO YA KIZAZI.
  3.  SARATANI YA MATITI
  4.  SARATANI YA NGOZI
  5.  SARATANI YA MAPAFU