Kisukari
Posted on: February 23rd, 2020Kisukari
Ugonjwa wa kisukari ni hali aambayo inatokea wakati sukari katika damu inakuwa nyingi kupita kiwango cha kawaida kwa muda mrefu. Ili mwili uweze kutumia sukari iliyotoka kwenye vyakula huhitaji kichocheo cha insulini. Insulin husaidia sukari kuingia kwenye chembechembe hai ili kutengeneza nishati-lishe.
Aina za kisukari
Kuna aina mbili kuu za kisukari ambazo ni;
- Kisukari kinachotegemea insulini
- Kisukari kisichotegemea insulini
Kisukari kinachotegemea insulini
Kisukari kinachotegemea insulin au “type one diabetes” husababishwa na upungufu au ukosefu wa kichocheo kinachotengenezwa kwenye kongosho kinachoitwa insulini.
Aina hii ya kisukari hudhibitiwa kwa kutumia sindano ya insulin kwani mwili huwa unashindwa kutengeneza kichocheo hiki, pamoja na kurekebisha ulaji. Mala nyingi aina hii ya kisukari huwapata watu wenye umri mdogo (watoto na vijana). Villevile mtu hawezi kurithi iwapo kuna historia ya kisukari katika familia.
Kisukari kisichotegemea insulin
Kisukari kisichotegemea insulin au “type two diabetes” husababishwa na mwili kushindwa kutumia sukari. Mwili wa mtu mwenye aina hii ya sukari huweza kutengeneza insulini ya kutosha lakini haitumiki kuuweesha mwili kutumia sukari na hivyo sukari katika damu huwa katika kiwango cha juu
Aina hii ya kisukari huweza kudhibitiwa kwa kutumia vidonge pamoja na kurekebisha ulaji; au kwa kurekebisha ulaji pekee. Mara nyingi huwapata watu wenye umri mkubwa kuanzia miaka 40 na kuendelea
Kumbuka
- Ufanisi wa tiba ya aina zote za kisukari hutegemea sana ulaji unaozingatia masharti yatolewayo na mtoa huduma za afya
- Muonekano wa mgonjwa wa kisukari kinachotegemea insulin mara nyingi huwa ni mwembamba wakati Yule mwenye kisukari kisichotegemea insulin huwa mnene.
Mambo yanayoongeza uwezekano wa kupata kisukari
- Uzito uliozidi (overweight) au unene uliokithiri (obesity)
- Kutofanya mazoezi
- Ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi
- Kuwa na shinikizo kubwa la damu
- Matumizi ya sigara na bidhaa nyingine za tumbaku
- Kuwa na umri wa zaidi ya miaka 40
- Historia ya kuwa na kisukari katika familia
Dalili za ugonjwa wa kisukari
- Kukojoa mara kwa mara
- Kusikia kiu sana
- Kusikia njaa sana
- Kuchoka sana na kukosa nguvu bila kufanya kazi
- Kutoona sawa sawa
- Kupungua uzito bila kukusudia
- Kusikia kizunguzungu
- Kuwa na maambukizi ya ngozi nz vidonda visivyopona upesi
- Baadhi ya viungo vya mwili kama vidole vya miguu na mikono kufa ganzi
Madhara ya kisukari
Ugonjwa wa kiskari usipodhibitiwa huleta madhara mbalimbali mwilini. Madhara haya huwa makubwa zaidi hasa pale mgonjwa anapokua hazingatii masharti ya matibabu na ulaji bora.
Kuna madhara ya muda mfupi na muda mrefu
Kushuka kwa kiwango cha sukari katika damu
Hali hii hutokea pale ambapo sukari hushuka kuliko kawaida. Hii inaweza kutokana na kutumia dawa kuzidi kipimo, kunywa pombe, kufanya mazoezi bila kula na kutokula kwa muda mrefu.
Dalili za kushuka kwa kiwango cha sukari katika damu
- Moyo kwenda mbio
- Mwili kutetemeka
- Kusikia njaa
- Kusikia kizunguzungu
- Kuona mbali (double vision)
- Kuchanganyikiwa
- Kutokwa jasho kwa wingi
- Kuchoka sana
Hali hii ikizidi mgonjwa huweza kupoteza fahamu na hatimaye kupoteza maisha kama hatapata matibabu mapema.
Kama mgonjwa akipatwa na hali hii asipewe kitu chenye sukari, ikiwemo glukosi, soda au juisi.
Kumbuka
|
|
Kupanda kwa kiwango cha sukari katika damu
Hali hii hutokea pale kiwango cha sukari kinapokuwa juu kuliko kawaida. Hii inaweza kutokea wakati mgonjwa anapoacha kutumia dawa, asipotunza dawa vizuri, asipotumia dawa kwa usahihi, anapoacha kufuata masharti ya ulaji unaotakiwa, anapopata maabukizo au maradhi mfano malaria, flu, nimonia nk
Dalili za kupanda kiwango cha sukari katika damu
Kupumua haraka haraka
Kukojoa mara kwa mara hasa wakati wa usiku
Kua na kiu au kukauka koo
Kunywa maji mengi
Kutoona vizur (ukungu)
Kuchoka bila sababu
Miguu na mikono kuchoma
Kizunguzungu
Kuongezeka mapigo ya moyo au moyo kwenda mbio
Kuchanganyikiwa
Kupungukiwa na maji mwilini
Kupoteza fahamu na hatimaye kupoteza maisha kama mgonjwa hatapata matibabu mapema
Kumbuka
Mgonjwa aliyepoteza fahamu asipewe chochote bali awahishwe katika kituo cha kutoa huduma za afya haraka sana
Madhara ya muda mrefu
- Upofu
- Maradhi ya figo
- Maradhi ya moyo
- Vidonda kutopona upesi na hatari ya kukatwa mguu
- Kufa ganzi na kupoteza hisia za mikono na miguu
- Kiharusi
Kuzuia kisukari
- Kula mlo kamili angalau mara tatu kwa siku
- Epuka kula chakula kingi kupita kiasi
- Epuka kula chakula chenye mafuta mengi au sukari nyingi
- Fanya mazoezi ya mwili mara kwa mara
- Pima sukarikatika damu mara kwa mara, angalau mara moja kwa mwaka
- Epuka matumizi ya pombe za aina zote
- Epuka matumizi ya sigara , bidhaa nyingine za tumbaku na madawa ya kulevya.
Jinsi ya kuishi na kisukari
Dhibiti ulaji wako
- Kula mlo kamili uliotayarishwa kutokana na angalau chakula kimoja kutoka katika kila kundi la vyakula
- Kula vyakula vya nafaka kama ulezi, mtama, uwele, ma nafaka zisizokoboewa kwa mfano dona, ngano, au shairi
- Kula mboga mboga kwa wingi kwa mfano mchicha, matembele, karoti, majani ya maboga, kisamvu, mlenda nk
- Kula kiasi kidogo cha vyakula vya nafaka, mizizi na ndizi katika mlo
- Kula vyakula vya jamii ya kunde kama mboga (sehemu ya mlo) kwa mfano maharagwe, njegere, mbaazi, kunde, choroko, nk
- Kula matunda kwa kiasi mfano ndizi au chungwa moja au kipande cha papai au embe kubwa katika kila mlo
- Kunywa maji kwa wingi
- Epuka ulaji wa vyakula vyenye sukari nyingi kama jamu, asali, chokoleti, pipi, bazooka, aiskrimu, na juisi bandia
- Epuka ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi
- Epuka unywaji wa pombe
Fanya mazoezi mara angalau nusu saa kwa siku
Tunza miguu yako kwa makini
- Epuka kuvaa viatu au soksi zinazo bana
- Epuka kuvaa viatu vyenye kisigino kirefu ambacho huweza kusababisha kuanguka na kuumia
- Osha miguu yako kwa maji safi na kausha vizuri hususan katikati ya vidole
- Usitembee bila kuvaa viatu
- Vaa viatu vya wazi na vyenye kisigino kifupi
- Epuka kijiumiza, na unapokua na kidondatibu mapema
Epuka msongo wa mawazo zingatia
- Afya ya kinywa kwa kupiga mswakiangalau mara mbili kwa siku
- Usafi wa mwili
- Taarifa a elimu kuhusu kisukari
- Taarifa na elimu kuhusu kisukari
- Masharti ya dawa na ulaji
- Kuhudhulia kliniki kama inavyoshauriwa
- Kumuona daktari mapema mara unapopata tatizo lolote la kiafya
Angalizo
- Awe makini na ulaji wake, hussani akiwa shuleni
- Azingatie na aoanishe muda wa kupata sindano ya insulin na muda wa kula
- Asaidiwe kuepuka kula vyakula visivyo bora kilishe
- Afikiriwe na aangaliwe wakati wa michezo, mazoezi, na kazi za kutumia nguvu
- Waalimu washirikiane n wazazi au walezi kuhakikisha motto anapata asusa zenye virutubishi muhimu anapokua shuleni